NISHATI YETU, MUSTAKABALI WETU

Na, G [Posted: 03/14/06]

Nadhani hatuhitaji kutumia muda kueleza suala hili maana mgawo wa umeme unaoendelea sasa hivi unatosha kabisa kuelezea tatizo hili. Na hili si tu kwamba linaathiri maisha ya kila siku ya wananchi, bali pia ni kikwazo kikubwa cha uwekezaji maana hata kama wawekezaji wanania ya kuwekeza nchini, ni vigumu kwao kufanya hivyo kutokana na ukosefu wa nishati ya kuaminika kuendesha mashine na mitambo yao ya uzalishaji, hivyo kusababisha wamue kuwekeza kwingine ambapo nishati inapatikana wakati wote na wala si kwa zamu.

Kwa minaajili hiyo basi, yawezekana wakati umefika kwa serikali kufikiri namna ya kuongeza vyanzo vya nishati maana kadri nchi inavyozidi kuendelea na idadi ya watu inavyozidi kuongezeka, ndivyo hitaji la nishati linavyozidi kuongezeka. Kwa hiyo kama uzalishaji wa nishati hasa ya umeme hauendani sambamba na ongezeko la hitaji la nishati hiyo, maendeleo ya nchi yatapooza kama si kulemaa.

Kwa miaka mingi Tanzania imekuwa ikitegemea nishati ya umeme wa nguvu za maji ambapo Siali (Turbines), zinawekwa katika maeneo ya maporomoko ya maji na kisha kuzungushwa na maporomoko ya maji hayo--Matokeo yake: umeme huzalishwa. Lakini baada ya muda na mahitaji kuongezeka na kupelekea ugunduzi wa gesi ya Songosongo, Tanzania ilipata nishati ya nyongeza ya kuzalisha umeme kutokana na gesi hiyo ya asili. Hili ni jambo la kujivunia kwa sasa maana taifa letu limekuwa moja ya nchi waasisi wa matumizi ya umeme wa gesi katika bara zima la Africa. Hii ni kwamba, hadi sasa mradi wa gesi ya songosongo unazalisha asilimia 45 (nusu) ya umeme wote unaotumika nchini. Ingawa hili ni jambo zuri, lakini wataalamu wa Songosongo wanadhani kwamba wanaweza kuzalisha umeme zaidi ya hapo kama wakiruhusiwa kuboresha uzalishaji wao. Kwa hiyo jambo la kwanza tunalokuomba mheshimiwa Rais/waziri wa wizara husika ni kutoa vibali vyote vinavyohusika, si tu kuwezesha mradi wa songosongo kuzalisha umeme kadri ya uwezo wao, bali pia kuhimiza utafiti wa upatikanaji wa vyanzo vingine vya gesi nchini ili kwamba kama vyanzo vingine vya kutosha vikipatikana, nchi iweze si tu kujitosheleza ki-nishati, bali pia kuuza nje nishati ya ziada.

Serikali pia inaweza kufikiria njia za kuelimisha watu wenye uwezo kuwekeza katika umeme unaotokana na miale ya jua (solar energy). Hii ni moja ya njia rahisi zaidi kwa serikali kufanya maana gharama yake ni nafuu mno. Kwanza, watu wenye uwezo wa kuwekeza inapaswa waelemishwe kufanya hivyo, kununua vifaa vya kukingia miale ya jua na kutengeneza umeme. Vifaa hivi ni ghali lakini faida yake ni kwamba ukishavinunua basi wewe unapata umeme wa bure nyumbani kwako siku zote. Ingawa labda ni wenye uwezo wachache wanaoweza kufanya hili, lakini kama wachache hao wakifanya, na kujiondoa kwenye gridi ya taifa, ina maana kutakuwa na ziada ya umeme ambao unaweza kutumiwa vinginevyo au na watu wengine. Kutegemeana na matumizi yao binafsi, wanaweza pia kuzalisha umeme wa ziada wa jua na kuiuzia gridi ya taifa hivyo kuongeza kiasi cha umeme unaogawanywa. Kitu cha pili serikali inaweza kufanya ni kufungua milango ya biashara na kuhimiza wafanyabiashara kuingiza vifaa hivi vya umeme wa miali ya jua kwakuondoa kodi ili watu waweze kumudu kuvinunua.

Makaa ya mawe nayo yanaweza kutusaidia kupata umeme. Sina hakika sana uwezo wa uzalishaji wa migodi yetu ya makaa kama Kiwira, na kwamba makaa hayo yanapopatikana yanatumiwaje. Lakini kama uzalishaji wa umeme si mojawapo ya matumizi hayo, basi tunaitia changamoto serikali kuwekeza katika teknolojia hii ya kuzalisha umeme kwa makaa ya mawe. Ingekuwa busara sana kuwekeza fedha kidogo kutafiti na kupanua uzalishaji wa makaa ya mawe nchini.

Chanzo kingine cha uzalishaji wa umeme ambacho kinazidi kupata umaarufu duniani, ni umeme wa njia ya upepo. Teknolojia yake inakaribia kufanana na ya umeme wa maji ila tu umeme wa njia ya upepo ambapo kunakuwa na makata-upepo makubwa ambayo yanawekwa katika maeneo yenye upepo na kuunganishwa na vitu vinavyokaribia kufanana na Siali (turbines). Hivyo upepo ukizungusha hizo kata-upepo, nazo kata-upepo zinazungusha Siali (Turbines)--matokeo yake, Siali zinazalisha umeme.

Asilimia 30 ya umeme unaotumiwa nchini Norway, unazalishwa kutokana na nguvu za upepo. Na upepo ni chanzo kizuri cha nishati kwani, tofauti na maji, upatikanaji wa upepo hautegemei uwepo wa mvua kwamba mazingira yakiharibiwa na kukiwa na ukame basi mvua zinakosekana na vina vya maji kwenye mabwawa ya umeme yanapungua, hivyo kuathiri uzalishaji. Upepo upo pale pale kama kuna mvua au jua, ukame au neema. Hadi sasa, kampuni inayoongoza kwa kuzalisha mitambo hiyo ya umeme wa upepo ni General Electric (GE) ya nchini Marekani. Hivyo, serikali inaweza kufikiria kuanza kununua mitambo hii na kuisimika maeneo mbali mbali nchini na kuongeza uzalishaji wa umeme, kuondoa kero ya kukatika kwa umeme nchini.

Ingawa hili ni jambo linaloleta malumbano makubwa toka kwa mataifa ya magharibi, lakini kulingana na mlipuko wa ongezeko la idadi ya watu, nadhani si dhambi kuanza kufikiria na labda kuanza utafiti utakaopelekea Tanzania kujiendeleza katika matumizi ya umeme wa ki-nuklia siku zijazo. Hiki ni chanzo kikubwa cha nishati ya umeme kwa nchi nyingi za magharibi (Ufaransa, kwa mfano). Na ni chanzo kizuri cha nishati kwani pamoja na maendeleo yao ya viwanda yanayohitaji matumizi makubwa ya umeme, pia maendeleo yao ya sayansi na teknolojia na wingi wa watu, tatizo la umeme kwa nchi hizo ni ndoto kabisa tofauti na ilivyo katika nchi zinazoendelea. Hivyo ingawa wanapiga kelele kuzuia nchi changa kujiendeleza katika nishati ya ki-nuklia, lakini nadhani kama nishati hii inawafaa wao, basi itatufaa na sisi pia. Kwa hiyo kazi ni kwako mheshimiwa Rais kuchukua hatua hii jasiri kuishawishi serikali ianze kuwekeza katika utafiti utakao-tuwezesha hapo baadaye kujiendeleza katika nishati ya ki-nuklia kukidhi haja ya umeme ya wananchi. Hata hivyo tunasikia tetesi kuwa kuna madini mengi ya Uranium huko Makutopora, Dodoma na katika nyanda za kusini mwa Tanzania (Mto Mkuju) yanayotosheleza kutokomeza kabisa tatizo la umeme nchini. Tunasikia kuwa tayari kuna mikataba ya kisirisiri inayofanywa na serikali kuyauzia makampuni ya kigeni miliki ya madini hayo adimu duniani. Moja ya makampuni hayo ni 'PLC' la Uingereza na 'GolStream' la Australia.

Tunaamini Mheshimiwa Rais utafanya kila lililo ndani ya uwezo wako kuakikishia kuwa nchi yetu inajitegemea kweye suala la nishati. Kila la heri katika kushughulikia hili pamoja na majukumu yako mengine yote.

Mungu Ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

Tuma maoni [Hapa>]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.