HUU SI UPINZANI BALI NI SIASA ZA KITOTO
Na, Antar Sangali - Bagamoyo
Kauli za hivi karibuni toka vinywani mwa baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani nchini Tanzania zinaweza kuudhihirishia umma kuwa viongozi hao aidha na vyama vyao kwa pamoja havina au hawana ukomavu katika medani za kisiasa na kidiplomasia.
Niliwahi kumsikia Mwenyekiti wa muda mrefu wa Chama Cha Democratic (DP) Mchungaji Christopher Mtikila akibeza kuendelea kwa mazungumzo kati ya CCM na CUF na kuwaita CUF ni wasaliti wa upinzani.
Lakini pia ikatoka kauli ya kumponda kiongozi mmoja wa CUF Bw. Hussein Mmasi akidai CCM na viongozi wa SADC hawaonyeshi kumkosoa Robert Mugabe na kwamba lao ni moja katika kufididi na kuififiisha demokrasia Afrika.
Dai la Mtikila ni kwamba katika kujadili mustakabali wa kisiasa nchini ni lazima vyama vyote vya siasa vihusishwe katika meza ya mazungumzo.
Katika siku chache zikatokea kauli nyingine toka kinywani mwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bw. Chacha Wangwe kwamba wao hawatambui muafaka utakaopelekea kuundwa kwa serikali ya mseto kati ya CCM na CUF huko Zanzibar...
Hakuishia hapo, Makamu huyo Mwenyekiti wa Chadema bila ya staha wala kuheshimu miiko ya kidiplomasia akathubutu kuwatupia lawama nzito wahisani wa serikali ya Tanzania kwa maana ya jumuiya ya Ulaya EU akitaka misaada yao isitishwe kwasababu kuna mafisadi.
Kiongozi mmoja aitwaye Bw. Kim wa EU akiwa katika mkutano huo kwenye ukumbi wa Karimjee hakusita kumpa ukweli Bw. Wangwe pale alipodiriki kusimama na kusema kuwa wanaridhika na upana wa demokrasia uliopo Tanzania na pia juhudi za kupambana na ufisadi zinavyochukuliwa.
Nimethubutu kusema kuwa baadhi ya viongozi na vyama vya upinzani bado vinasuasua katika kufikia upeo halisi wa kutoa mizungu ya kisiasa na diplpomasia kutokana na kauli hizi zilizokaa katika umbile la mshazari toka kwa wakubwa hawa wanaotazamiwa kuwa mbadala wa uongozi wa CCM ikiwa wananchi wataamua kwa makasha ya kura.
Nijuavyo mimi chama cha siasa ni uwakilishi wa wazi wa wanachama na kazi za chama hicho kisiasa katika mfumo na mtandao mmoja wenye kujenga itikadi moja, sanjari na mwelekeo wa sera.
Chama cha siasa si kupata tu hati ya usajili kwa msajili wa vyama vya siasa kwa mujibu wa sheria No. 5 ya mwaka 1992 hapa nchini bali ni ufanyaji wa kazi hizo katika uwazi wa demokrasia kadri inavyohitajika.
CUF ni chama kikubwa cha upinzani Zanzibar, kina uwakilishi wa wanachama katika medani za kisiasa na pia kina wawakilishi na wabunge katika uga wa kiserikali, kimsingi kina uwezo wa kushirikishwa na kudai kushirikiana katika mazingira yoyote tata na tete.
DP hakina hata mwenyekiti wa Mtaa au kijiji, hatuoni kikifanya hata mkutano mkuu, kamati kuu, au kamati ya utendaji na wajumbe wa kamati hizo au kwa aina nyingine ya majina hayafahamiki hapa nchini.
Uko wapi uwakilishi na ushirikishwaji wa chama hiki ambacho msemaji, sera, itikadi na misimamo ni kauli za mwenyekiti kila kukicha. Iko wapi safu ya uongozi wa DP toka kilipoanzishwa kama si makovu ya kufukuzana kwa kila anayempinga Mwenyekiti?
Mtikila anapojitutumua ati ashirikishwe yeye na DP kwa maslahi ya nani katika dhana ya ushirikishwaji au ni ubutu katika kufikiri na kuleta ufisadi katika kuifikia dhamira njema inayoweza kufungua ukurasa mpya wa historia katika nchi hii.
Hivi kauli ya CUF kupitia kwa Bw. Mmasi akiwa katika mkutano hapa Bagamoyo inafanana na ukweli kuhusu Rais Jakaya Kikwete na jitihada zake za kukutana na kiongozi wa MDC cha Zimbabwe Bw. Morgan Tshangarai kwa falagha huko Adis Ababa, anatambua alichozungumza au ni kubwabwaja kama yuko katikajukwaa la kisiasa.
Najiuliza mara nyingi zaidi kwa kila kitu kifanywe katika sura ya kisiasa na je wanaitambua diplomasia inapoweza kuisaidia kuleta suluhu hata panapo na vita kali!!
Najiuliza mara nyingi zaidi hivi ilikuwa ni sahihi Bw. Wangwe akikataze chama cha CUF kisiafikiane na CCM katika kufikia serikali ya Mseto huko Zanzibar,? au pale anapodai kwamba hawaiungi mkono CUF katika kuunda serikali ya mseto na CCM bali ni lazima ing”oke tu madarakani! maswali yote haya sipati majibu haraka.
Wakati viongozi wa upinzania Tanzania wakitoa matamshi haya katika mahojiano yangu na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Mzee Pius Msekwa anasema utaratibu wa kwamba chama kinachoshinda kiunde serikali peke yake ni kuzusha rabsha Afrika.
Msekwa amezitolea mfano nchi za commonwealth kwamba ndizo zenye katiba zenye vigingi hivi jambo ambalo amedai ni kinyume na matakwa ya wengi kuligana na mabadiliko ya wakati katika dunia ya leo.
Mzee Msekwa akaaenda mbali na kusema hilo wao CCM wamelibaini katika kikao chao kilichoketi Butiama kwamba ipo haja ya kuulizwa wazanzibar juu ya hatma ya uongozi katika medani za utawala ili serikali ya ubia iundwe.
Makamu huyo Mwenyekiti wa CCM anatamka kuwa mfano mzuri ni wa Mzee Nelson Mandela na ANC mwaka 1994 licha ya kushinda kwa ushindi mpana aliamua kuwashirikisha wapinzania serikalini.
Matamshi yote haya ya Msekwa inaonyesha CCM ni jinsi gani inavyotaka kucheza karata za mapiku katika kujenga na kufikia ukweli huku viongozi wa upinzani wakibaki katika tahayuri nzito ya kupayuka bila mizania na nadhari.
Uamuzi pia wa CUF kuyasuasia mazungumzo si sahihi kwasababu wao viongozi ni wawakilishi wa wanachama na nje ya wanachama wao wako ambao si wanachama ambao kwao pengine wanaihitaji kwa udi na ambari fursa na njia ya kura ya maoni ili kuifikia dhamira.
Kwanini wasite na kuhofu, huo ni ubutu na kitete mithili ya utoto zaidi katika siasa za ushindani.
Kwa upinzania huu na matamshi haya ya pupa ya kipovu cha mdomo iko kazi kwelikweli ya kuiondoa CCM na kujipa uhalali mbele ya umma kama vyama na viongozi wa upinzani mmepata utayari.
Mungu ibariki Afrika.
TUMA MAONI YAKO [HAPA]