WATOTO WA MAMA TUNAIANGAMIZA TANZANIA

Na, Magabe Kibiti<posted: 09/24/06>

Ni karibu saa tano asubuhi jijini Dar es salaam ingawa joto ndani ya chumba cha mikutano katika ofisi ya waziri mkuu wa Tanzania (Mhe Sumaye) linazidi kupanda kwa kasi ya ajabu. Kinachoendelea hapa ndani ni mkutano kati ya viongozi wa wanafunzi wa vyuo vya juu nchini na Mhe Sumaye. Kuna mambo mengi sana kwenye ajenda lakini kuna muda mfupi sana wa kuyajadili kwa sababu ratiba ya waziri mkuu inazidi kubana kadri uchaguzi mkuu (2000) unavyokaribia. Cha kufurahisha na kuumiza ni tofauti kubwa sana iliyopo kati ya msimamo wa wanafunzi na serikali. Wanafunzi wanataka waongezewe pesa za posho na bajeti ya serikali kwenye elimu ya juu, huku Mhe Sumaye akisisitiza kuwa serikali haina uwezo huo. Kikao kinamalizika bila muafaka na viongozi wa wanafunzi wanarudi kampasi kuendelea na mgomo.

Huu mgomo sio wa kwanza na kadri jaribu la nyakati (test of times) litakavyothibitisha, migomo ya wanafunzi wa elimu ya juu imeendelea na inaendelea kufanyika. Mwonekano kuwa hakuna mwisho wa hii migomo, na kauli zinazopingana za viongozi wa serikali kuhusu elimu ya juu na huduma nyingine za jamii; vimepelekea uandishi wa makala hii. Sio sifa au kujitakia umaarufu ila ukweli kwamba mimi ni miongoni mwa waliowawakilisha wanafunzi kwenye kikao na Sumaye, ni moja ya sababu zinazonishawishi niendelee kuandika makala hii. Sio uongo, mimi kama vijana wengi ninaowafahamu wa kizazi changu na hasa wale tuliokuwa mbelembele kwenye mgomo, tulikuwa tukidai kuwa ni jukumu la serikali kufanya kila kitu ili kutuletea maendeleo. Hii inaweza kuwa imesababishwa na ukweli kuwa tulikuwa tumeona kwa macho yetu baadhi ya wananchi wenzetu wanaofanya kazi serikalini wakiishi maisha kama wako peponi.

Kwa miaka karibu mitatu nilokuwa pale chuoni, nilishuhudia baadhi ya wadosi wa chuo wakibadilishiwa mashangingi (magari ya fahari) kila mwaka na kukatiwa mishiko ya nguvu na serikali. Hii pamoja na mambo mengine, ilipekea mimi kuamini kuwa serikali yetu ilikuwa na uwezo mkubwa sana wa kipesa. Mtazamo huu wa maisha, ulipelekea mimi na baadhi ya wenzangu kuukubali udhaifu wa kuishi kama watoto wa mama. Maisha yaliyopelekea tuishi na kusoma chuoni tukitegemea kila kitu kufadhiliwa na serikali. Sio nia ya makala hii kusema kwa hakika kama kitendo cha kushiriki katika mgomo huo kilikuwa halali au haramu. Ajenda kubwa hapa ni kujaribu kuchambua kwa kina uhalali wa kuishi maisha ya kutegemea kila kitu kutoka serikalini au kwa wafadhili. Ninaongelea maisha ya mtoto wa mama hapa. Maisha ya mtoto ambaye kila kitu anategemea mzazi wake amfanyie bila ya yeye mwenyewe kujishughulisha hata kidogo tu kubadili mwelekeo na mwafaka wa hali ya mambo yake muhimu .

Kama ilivyotegemewa, mgomo huo haukuwa na mwisho mzuri hasa kwetu sisi viongozi wa serikali za wanafunzi. Ninachokumbuka ni kuwa moja ya siku zilizofuata nilijikuta selo ya sarenda. Baadaye nilijikuta Amerika ambako nilitakiwa niishi maisha ya kusubiri king'ora cha saa yangu kilie saa tatu na nusu usiku ili kuniamsha niende kazini ambako nitafanya kazi ya kufunga magaloni ya gesi kwa masaa manane mfululizo. Baada ya hapo nitatakiwa kuripoti kwenye kazi yangu ya pili ambako nitaamsha, kuosha, kuvalisha, kulisha, kuchambisha, kulaza, kuamsha tena, kulisha, na kulaza wazee wa kizungu zaidi ya kumi kwa masaa manane mfululizo yanayofuata. Baada ya hapo, takribani saa tisa mchana, nitatakiwa kwenda shuleni kusikiliza mhadhara kwa masaa matatu yanayofuata. Mnamo saa kumi na mbili na nusu jioni, ninategemea kurudi nyumbani nijaribu kulala kwa masaa mawili au matatu kabla ya kuamshwa tena na king'ora cha saa yangu saa tatu na nusu usiku na kuanza tena mzunguko wote nilioueleza hapo juu.

Usipokuwa mvumilivu utaanza kubeza uamuzi wa kutumia mfano wa maisha ya marekani katika makala hii. Nia kubwa ya makala hii ni kuonyesha tofauti kubwa ya maisha na mtizamo wa maisha, mshituko wa moyo, mabadiliko ya fikara, ushawishi wa maamuzi, na utafsiri wa nafsi unaotakiwa kujenga au kubomoa maisha ya sasa na ya baadaye ya Mtanzania. Ajenda kubwa hapa ni kujaribu kuchambua kwa kina uhalali wa kuishi maisha ya kutegemea kila kitu kutoka serikalini au kwa wafadhili. Ninaongelea maisha ya mtoto wa mama hapa. Maisha tuliyooishi chuoni tukitegemea kila kitu tufanyiwe na serikali. Nadhani msomaji umejenga picha ya mshtuko nilioupata nillipofika Marekani ambapo nilitakiwa kufanya kazi masaa kumi na sita kila siku ili kulipia shule, nyumba, chakula, umeme, na gharama nyingine za maisha ya marekani.

Raisi wa zamani wa Marekani hayati John Kennedy aliwahi kusema maneno yaliyomfanya ahesabike miongoni mwa viongozi mashuhuri sana walioingoza Marekani. Katika hotuba yake ya kukabidhiwa uongozi, Kennedy alisema yafuatayo: Usijiulize ni nini unategemea kufanyiwa na serikali, jiulize ni nini utaifanyia serikali na nchi yako . Huu ndio ukweli ambao wamarekani wengi wamekuwa wanauishi kwa muda mrefu sasa. Ingawa serikali ya marekani inasifika duniani kwa juhudi zake za kumkomboa raia wake yeyote anayepatwa na matatizo makubwa ndani na nje ya nchi, wamarekani wengi sana wanahangaika kujua nini wafanye ili waisaidie nchi yao. Hali ndio hii hii hata kwa raia wa mataifa mengine tajiri duniani. Ingawa nimekuwa miongoni mwa watu wengi wanaopinga tabia ya kuiga tamaduni za kizungu au za kiarabu na kuzileta Tanzania, wakati huu ninaomba nipingane kidogo na marafiki zangu katika jambo hili. Utamaduni wa kuishi maisha ya kutoitegemea serikali kwa kila kitu una manufaa kuigwa. Ninashauri kuachana na maisha ya utoto-wa-mama. Watoto wa mama tunaliangamiza taifa letu la Tanzania.

Ni kweli kwamba serikali ina majukumu yake muhimu ya kuandaa sera nzuri zenye uwezo wa kuwaletea wananchi wengi maendeleo. Ni kweli pia kuwa ni jukumu la serikali kuweka msingi imara ambao utapelekea upatikanaji wa huduma muhimu za wananchi kama maji safi, nishati, huduma za elimu na afya, malazi, mawasiliano ya uhakika, uongozi bora, na utawala wa sheria. Ni ukweli usiopingika hata hivyo kuwa; ni jukumu la wananchi (binafsi au kwa ushirika) kutekeleza majukumu yao ya kuiletea Tanzania na hatimaye Afrika nzima maendeleo. Makala hii inalaani vikali suala la baadhi ya viongozi serikalini kuishi pia kama watoto wa mama kwa kutegemea kuwa maisha yao yataendeshwa kwa rushwa, ubadhirifu, na unyonyaji wa uchumi wa watanzania wenzao. Makala hii inalaumu pia suala la baadhi ya vijana Tanzania kukaa vijiweni bila kufanya kazi yoyote huku wakiilalamikia serikali kwa kutowapatia ajira. Makala hii inashauri wanafunzi wa vyuo vikuu na wasomi nchini kutafuta mbadala wa sera ya sasa ya kusoma kwa kutegemea serikali na wafadhili kugharimia kila kitu muhimu katika mafanikio ya elimu. Ni wakati muafaka sasa wa kuachana na maisha ya utoto wa mama.

Makala hii imetumia tu mfano hai wa maisha binafsi kusisitiza pointi ya kuachana na maisha ya utoto wa mama. Kumbuka ndugu msomaji kuwa nimetumia neno tuachane kwa sababu hata mimi nimewahi kuwa na mawazo haya ya kuishi maisha ya utegemezi. Nimeamua kuachana na utoto wa mama. Nimechoshwa na kauli za viongozi vihiyo serikalini wanaosingizia ukosefu wa pesa za kigeni na ufadhili kwenye vitu hata vya msingi walivyoshindwa kuifanyia nchi yao. Ni aibu kwa viongozi hawa kuishi maisha ya utegemezi kama watu binafsi, na kisha kuifanya nchi nzima iishi maisha hayo hayo ya utoto wa mama. Nina imani kuwa serikali mpya ya Kikwete itajaribu kubadili hali ya mambo na kuwaondoa watoto wa mama kutoka serikalini, kuachana na utegemezi usio wa lazima wa misaada ya nje, na kuwakumbusha wananchi kuwa ni jukumu lao kuisaidia nchi na sio kusaidiwa na nchi.

Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

 

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.