TATHIMINI YA UCHAGUZI MKUU 2005:KWANINI UPINZANI HAUKUFANYA VIZURI?
Na, BongoTz <04/12/10 >
Kama ripoti ya Profesa Mukandala ilivyowahi kuonyesha siku za nyuma, vyama vingi nchini Tanzania bado vinalegalega na wala havijui viendako. Sote tumeshuhudia kufanya vibaya kwa vyama hivyo kwenye uchaguzi mkuu uliopita (Disemba 14, 2005) kuliko hata ilivyokuwa katika chaguzi mbili za nyuma (mwaka 1995 na mwaka 2000).
Kando na kutokuwa na sera za kueleweka, migogoro ya muda mrefu baina ya vyama na ndani ya vyama vyenyewe, ufinyu wa elimu ya uraia kwa wanachama wa vyama hivyo, pamoja na kutobadilika kwa wagombea wa nafasi za juu na kusimamisha utitiri wa wagombea; . ni baadhi tu ya sababu za msingi zilizofanya vyama hivyo kufanya vibaya katika uchaguzi wa mwaka huu.
Mtu mwenye akili timamu atakaa chini na kufikiri kuwa, baada ya chaguzi mbili zilizopita, upinzani ungekaa pamoja na kufikia uamuzi wa pamoja wa jinsi ya kukikaili Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi wa Desemba 14, 2005; lakini badala yake, kila chama kilidhani kina ubavu wa kupambana na CCM ambayo imekuwa madarakani kwa zaidi ya miongo minne. Kila chama kikaamua kujitupa ulingoni kivyakevyake kwa matumaini bandia kuwa muujiza utatokea hivyo kuing'oa CCM madarakini.
Wapinzani kwa ufinyu wao wa kufikiri, kuona, na kusoma maoni ya Watanzania, wakajiona wanakubalika mbele ya jamii. Lakini uroho na uchu wao wa madaraka ukageuka kuwa bakora kali dhidi yao.
Athari za migogoro katika vyama vya siasa nazo zilichangia: Kwa ujumla wake migogoro mikubwa iliyoanza kuitiksa kambi ya upinzani mwishoni mwa miaka ya tisini na kuendelea hadi uchaguzi mkuu wa 2005 ilichanga kudorora kwa vyama hivyo vya upinzania na hivyo kusababishakufanya vibaya. Tumeshuhudia mgogoro mkubwa wa kugombea madaraka ndani ya UDP ambapo kamati kuu ya chama hicho ilitimua Mwenyekiti Bwana John Cheyo, na baadaye ikafuatia timua-timua. Athari zake ni kwamba: baadhi ya wabunge waliotuhumiwa kushirikiana na Bwana Amani Jidulamabambasi kumpindua Mwenyekiti wakawa wa kwanza kutimuliwa. Matokeo: Aliyekuwa Mbunge wa UDP na Madiwani 9 walihamia CCM na wanachama 1,147 wa wilaya ya Bariadi walihamia CCM pia. Tumeshuhudia kitu hicho hicho ndani ya TLP na NCCR -MAGEUZI pia.
Kutokana na migogoro kushamiri ndani na baina ya vyama vya siasa, wananchi walio wengi wamefikia hatua ya kuondokewa kabisa na matumaini dhidi ya vyama hivyo. Na mwaka huu wameamua kutoa tamko kali ambalo ni Kura ya “HAPANA."
Kwa upande mwingine, ufinyu wa elimu ya uraia kwa wanachama wengi wa vyama vya upinzani umechangia kwa kiwango fulani kuvikosesha vyama hivyo kura halali. Mfano, wadadisi wa mambo ya kisiasa wanadai kuwa wananchama wengi wa chama cha CUF waliongozwa na jazba zaidi kuliko hekima. Mathalani, badala ya kupiga kura ya "HAPANA" kwa mgombea wasiyemtaka, wengi wao waliishia kuandika matusi na maneno ya kejeli mbele ya picha za mgombea. Matokeo yake: kura hizo zilihesabiwa kama zimeheharika.
Kando na kutokuwa na sera za kueleweka, kutobadilika kwa wagombea wa nafasi za juu na kusimamisha utitiri wa wagombea ni sababu nyingine za msingi zilizofanya vyama hivyo kufanya vibaya katika uchaguzi wa mwaka huu. Vyama vya upinzani bado havijajikita mizizi vijijini, wala havijajulikana sana ukiachilia mbali sifa za waanzilishi wake. Majina ni yale yale ya akina Mrema na Lipumba. Wananchi wamewachoka!
Mpaka hapo vyama vya upinzani vitakapojipanga upya na kujua kuwa, njia mbili kubwa za wao kushinda uchaguzi ni: [moja] kuhakikisha kuwa wanasimamisha mgombea/wagombea chini ya kivuli cha chama chenye nguvu na mvuto--kama ilivyo CCM hivi sasa. Maana yake ni kuwa hata kama mgombea atakuwa hovyo kiasi gani, atabebwa na kuchachaguliwa kwa sababu tu ya nguvu na mvuto wa chama anachowakilisha. Njia nyingine na ya pili ni mgombea mwenyewe kuwa na sifa ambazo zinatosha kuvutia wananchi wampigie kura, na sio chini ya kivuli cha chama chake tu.
Pamoja na kelele zote za wapinzani kuwa serikali inapendelea chama tawala, bado chama tawala kitaendelea kushinda na kuisabaratisha ngome ya upinzani sikuzote hadi hapo kitakapopatikana chama chenye upinzani wa kweli na nguvu ya siasa. Na sio nguvu ya siasa tu, bali pia sera zinazoeleweka.
Lakini bado haijafikia wakati chama tawala kikakosa usingizi kwa kuhofia kupoteza madaraka kwa upinzani. Bado sana! Na kwa mtaj huo basi, uchaguzi ujao mwa 2010 matokeo ni: CCM "1", MAGEUZI "0".
Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!
Tuma maoni [Hapa>]